Chenge aivimbia tume.

Baraza la Maadili la Watumishi wa Umma jana lilishindwa kumhoji Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, baada ya kuwasilisha pingamizi la amri ya Mahakama Kuu inayodaiwa kuzuia mamlaka zozote kujadili au kulifanyia kazi suala lolote linalohusu kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji kifisadi wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Zuio hilo lilizua mvutano mkali wa kisheria baina ya wanasheria wa baraza hilo na Chenge, ambaye alilitadharisha kutokubali kuingia kwenye siasa, badala yake waiache majukwaani na washughulikie masuala ya msingi kisheria.

Chenge alidai ana maelezo ya kutosha ya tuhuma zilizoorodheshwa na baraza hilo dhidi yake, lakini kabla ya kuanza kujieleza ni vyema akapata mwongozo.
Mvutano huo ulizuka muda mfupi baada ya Mwanasheria wa Baraza hilo, Hassan Mayunga, kusoma hati yenye malalamiko 10 dhidi ya Chenge, yakiwamo ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Umma tangu akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 1995.
Baada ya kusomewa malalamiko hayo, Chenge aliomba mwongozo wa baraza akidai kuna zuio la mahakama kwa mamlaka zozote za serikali kushughulikia suala hilo.
MVUTANO ULIKUWA HIVI
“Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo. Malalamiko dhidi yangu chimbuko lake ni maamuzi ya Bunge katika mkutano wa 16 na 17. Ninavyofahamu mimi suala hili lipo mbele ya Mahakama Kuu na uamuzi umeshatoka kuwa mamlaka yoyote hairuhusiwi kushughulikiwa kwa namna yoyote ile,” alisema Chenge.

Aliongeza: “Hii ni ‘public document’ (waraka wa umma) bila mwongozo huo, mimi kama mwanasheria inanisumbua sana.”
Baada ya kauli hiyo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu, Hamis Msumi, aliomba kuona zuio hilo.
Jaji Msumi: Naomba hilo zuio nilione…nimelisoma kwa uchache, je mnalo hili?
Mwanasheria Mayunga: Nimelisoma na halituzuii kuendelea na malalamiko yetu dhidi ya Chenge. 
Mayunga alipinga mwongozo huo na kudai zuio la mahakama halihusiani kwa namna yoyote na malalamiko yaliyo mbele ya baraza dhidi ya Chenge.
“Tuhuma zilizopo mbele ya baraza ni ukiukwaji wa sheria na kanuni za maadili ya viongozi wa umma na siyo suala la kinachoendelea na kilichoelezwa katika zuio hilo, hivi ni vitu viwili tofauti,” alifafanua.
Mayunga alidai kwa mujibu wa Ibara ya 132 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sekretarieti ya Maadili ya Watumishi wa Umma inatajwa ikiwa  na mamlaka kamili ya kuhoji na kwa msingi huo iko huru na haipaswi kuingiliwa.
Alifafanua kuwa Sheria ya Maadili kifungu cha 18 (2) (c) inaeleza majukumu ya sekretarieti ambayo ni kuchunguza madai yoyote ya uvunjaji wa sheria ya maadili.

Mayunga alidai kuwa kifungu cha 4 kinatoa mamlaka kwa sekretarieti kuanzisha uchunguzi na ukiukwaji wowote wa maadili kulingana na matakwa ya sheria.
Alisema kifungu namba 29 cha sheria hiyo pia kinaeleza hakuna chombo kinachoweza kupunguza au kuzuia kufanya kazi yake na kwamba kwa vifungu hivyo Baraza hilo liko sahihi kuendelea na shauri hilo. Baada ya ufafanuzi huo, Chenge alisema anachofahamu hoja aliyoiwasilisha mbele ya baraza ni zuio lililopo Mahakama Kuu na kwamba iwapo chombo hicho (Baraza) kipo juu ya Mahakama hilo ni jambo jingine.
Hata hivyo, alitakiwa kusoma kipengele kimojawapo cha zuio hilo na kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili na alifanya hivyo huku akisisitiza moja ya kipengele ni kuhusu miamala ya benki iliyofanyika.
“Nionavyo chombo hiki (Baraza) kiheshimu amri halali iliyotolewa na Mahakama…unapokuwa katika hali kama hii Mamlaka ya chombo hiki yasiwe makubwa kushinda Mahakama Kuu…ni ushauri tu unaweza kuendelea kunihoji na maelezo ninayo ya kutosha,” alisema. 
Aliongeza: “Utawala wa sheria uheshimiwe, masuala ya siasa yabakie kwenye majukwaa mengine yasiingizwe kwenye chombo hiki.”
“Kilichotajwa kwenye malalamiko dhidi yangu ni miamala ya benki ambayo imetajwa katika zuio la Mahakama, tusijifiche katika kichaka cha kusema sheria ya maadili inafanya kazi, suala hili lilianzia bungeni,” alisisitiza.
Mwanasheria wa Baraza, Filoteus Manula, alidai suala la ukiukwaji wa maadili haliendani na mashauri kama ya jinai, madai na rushwa, na kwamba kinachozungumziwa kwenye malalamiko ni ukiukwaji wa maadili aliyoyafanya tangu akiwa na wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa serikali. Mwanasheria mwingine wa Baraza, Getrude Cyriucus, alidai kuwa sekretarieti hiyo imepewa mamlaka ya kuanzisha uchunguzi bila kusubiri na wapo huru kuanzisha kuchunguza kupitia taarifa mbalimbali ikiwamo vyombo vya habari.
“Tukiacha viongozi wa umma wajichagulie watakavyo, kamwe hatuwezi kufanya kazi yetu inavyotakiwa,” alidai.
Baada ya mvutano huo wa dakika 30, Chenge alisema alichoomba ni mwongozo na kuwasilisha mbele ya baraza zuio la mahakama, hivyo waamue kama wataendelea au la na kwamba ana maelezo ya kutosha dhidi ya tuhuma zilitotolewa dhidi yake.
MALALAMIKO DHIDI YA CHENGE 
Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 1995, aliishauri serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na Kampuni ya Independent Power Solution Limited (IPTL) wa kuongeza uzalishaji wa umeme.
Pili, baada ya kustaafu wadhifa wake huo, Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006, aliingia mkataba wa kuwa Mshauri Mwelekezi (Consultant) wa Kampuni ya VIP Engineering  and Marketing Limited iliyokuwa na hisa za asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL.
Tatu, kitendo cha mlalamikiwa (Chenge) kuingia mkataba na kampuni hiyo ya VIP iliyokuwa na hisa na kampuni ya IPTL ni ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, kifungu cha 6 (j) ambacho kinazuia kiongozi wa umma kujinufaisha utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata alipokuwa anatekeleza majukumu yake kwa manufaa binafsi.
Nne, kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri mwelekezi wa Kampuni ya VIP akiwa na wadhifa wa ubunge, ni ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 6 (e) ambacho kinazuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa kimaslahi.

Tano, mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na VIP ulimpatia manufaa ya kifedha ya Sh. bilioni 1.617 kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu 12 (1) (e).
Sita, Chenge aliingiziwa fedha hizo Februari 5, mwaka 2014 katika akaunti yake 00120102523901 iliyopo kwenye benki ya Mkombozi, tawi la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam.
Saba, kitendo cha mlalamikiwa kuingia mkataba na Kampuni ya VIP ambayo ilikuwa na hisa na IPTL aliisaidia kujipatia manufaa ya kifedha kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 12(1) (e).
Nane, mlalamikiwa hakutamka maslahi aliyonayo katika mkataba na VIP aliyoingia nayo mkataba mwaka 2006, kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 15.
Tisa, mlalamikiwa hakutamka maslahi aliyokuwa nayo katika mkataba wa Tanesco na IPTL kupitia VIP kinyume cha fungu la 18 la sheria ya maadili.
Kumi, mlalamikiwa hakutamka madeni yake aliyokuwa inaidai kampuni ya VIP kwa kamishna wa maadili kinyume cha matakwa ya kifungu la 9 (6) ya sheria ya maadili ya viongozi ya umma.
KAULI YA BARAZA
Baada ya baraza kusikiliza mvutano huo, Jaji Msumi alisema watakwenda kusoma zuio hilo kwa kina na kutoa maamuzi leo.
“Najua tuna madaraka, lakini kama kuna zuio la Mahakama Kuu basi baraza haliwezi kuendelea na suala hili kwa kuwa haliko juu ya sheria,” alisema.
MALALAMIKO YA WANASHERIA
Baada ya Mwenyekiti kuahirisha kikao hicho, wanasheria wa baraza hilo walilalamika mbele ya waandishi wa habari kuwa walisoma zuio hilo kabla ya kuandaa malalamiko dhidi ya Chenge na nakala waliyokuwa nayo ina kurasa tatu, lakini iliyowasilishwa na Chenge ina kurasa saba, jambo ambalo halieleweki.
Kikao cha baraza hilo litaendelea leo kwa kutoa mwongozo kwa ombi la Chenge. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa awali na Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma, ilionyesha kuwa baada ya Chenge atamfuata aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja, Mkurugenzi wa Sheria, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma na Mnikulu Shaban Gurumo.
KWA NINI CHENGE ANAPINGA
Chenge anapambana dhidi ya tuhuma mbele ya baraza kwa kuwa ikithibitika kuwa alikiuka maadili, anaweza kuathirika kisiasa hasa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, kushindwa mbele ya baraza kunaweza kuibua kesi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba alikwepa kodi, hivyo kuingia kwenye mgogoro wa kikatiba. 
Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 67 (c) inataja mambo yanayoweza kumpotezea mtu sifa ya kuwania ubunge kuwa ni kutiwa hatiani kwa kukwepa kodi ya serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kushindwa mbele ya baraza kunaweza kuwa mwanzo wa kesi hiyo.
CHANZO: NIPASHE
Previous
Next Post »