Mtoto huyo, Yohana Bahati, mwenye umri wa mwaka mmoja, aliibwa
usiku wa kuamkia jana, akiwa amebebwa na mama yake, Esther Bahati (30),
ambaye alivamiwa na watu hao na kupigwa mapanga akiwa jikoni kisha
kuporwa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alisema tukio hilo
la kusikitisha lilitokea juzi saa 2:00 usiku, wakati mama huyo akiwa
jikoni anapika chakula na watu hao kumvamia na kumkata mapanga sehemu
mbalimbali za mwili wake.
“Watu wasiofahamika walimjeruhi mama wa mtoto kisha kumtwaa
mgongoni pasipo kumdhuru na kutoweka sehemu isiyojulikana mpaka sasa
hajapatikana wakati jeshi la polisi likiendelea kuwasaka waliotenda
uhalifu huo,” alisema Kamanda Konyo.
Konyo alisema Esther baada ya kujeruhiwa kwa mapanga, aliwahishwa
na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya kupatiwa
matibabu baada ya kujeruhiwa usoni, mikononi na mabegani alipokuwa
akijaribu kupambana na watu hao wasimchukue mwanaye.
Alisema kutokana na tukio hilo, polisi mkoani Geita inamshikilia
baba wa mtoto huyo, Bahati Misalaba, ambaye wakati tukio hilo linatokea
alikuwa akiota moto nje ya nyumba hiyo.
Hata hivyo, Konyo alisema polisi wameimarisha ulinzi katika nyumba
ya familia hiyo kutokana na kuwapo watoto wengine wawili albino ambao
wakati tukio likitoe walikuwa wakicheza nyumba ya jirani.
Kamanda huyo alisema baba wa mtoto huyo, Misalaba, wakati tukio
linatokea, alikuwa akiota moto maarufu ‘kikome’ nje ya nyumba hiyo.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha siku 51 kutokea tukio kama
hilo baada ya mtoto Pendo wa kijiji cha Ndami, wilaya ya Kwimba, mkoani
Mwanza, kutekwa na watu wasiofahamika, huku jeshi la polisi likiendelea
kuwasaka waliotenda uhalifu huo pamoja kumtafuta Pendo akiwa hai ama mfu
bila ya mafanikio hadi sasa.
Juhudi za jeshi hilo na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa
Mulongo, kutaka mtoto huyo apatikane ndani ya siku tano, ziligonga mwaka
kwa kipindi hicho licha ya polisi kuendelea na msako na upelelezi kwa
watu nane inaowashikilia akiwamo baba wa Pendo, Emmanuel Shilinde.
TAKWIMU ZA KIMATAIFA
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, asilimia mbili ya watu
wanazaliwa na ulemavu wa ngozi husherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwao,
wakati barani Afrika mtu mmoja kati ya 2,000 huzaliwa akiwa albino
tofauti na Marekani ambako mtu mmoja kati ya 17,000 huishi wakiwa wa
ulemavu wa ngozi.
Mauaji na albino nchini yanaonekana kushamiri hususani katika mikoa
ya kanda ya ziwa kutokana sababu kubwa za imani za kishirikina ambazo
pia zinasababisha mauaji ya vikongwe tangu yalipoanza mwaka 2006/2007.
UNDER THE SAME SUN
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kuwalinda watu wenye ulemavu wa
ngozi (albino), Under the Samesun (UTSS) lenye makazi yake nchini
Canada, Peter Ash, alishangazwa na vyombo vya dola nchini kushindwa
kuwakamata wanunuzi wa viungo vya albino licha ya kutajwa na waganga wa
kienyeji na wauaji wenyewe.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza hivi karibuni, Ash
alisema viungo vya albino vinanunuliwa kwa bei kubwa ambayo mwananchi
wa kawaida hawezi, hivyo vyombo vya dola vinapowakamata wauaji na
kuwahoji na kuwaelekeza wanunuzi, vinashindwa kuwakamata.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon