Wachezaji saba Simba waibua mapya

SIMBA inapambana kiume kurejea kwenye ubora wake, lakini wachezaji saba wameibua mapya na kuumiza vichwa vya wanachama na viongozi kwa vile mikataba yao ni tatizo.

Nyota hao wapo hatarini kutimka kwenye kikosi hicho kutokana na mikataba yao kubakiza muda mfupi wa kuitumikia timu hiyo na kwa mujibu wa taratibu za usajili, kwa sasa wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu nyingine ingawa kusajiliwa ni mpaka usajili ufunguliwe.
Wachezaji hao ni Said Ndemla ambaye wakati wa usajili wa dirisha dogo alikuwa akihusishwa na Azam FC, William Lucian ‘Gallas’ na Abdallah Seseme ambao kwa sasa hawapewi nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kocha Goran Kopunovic.
Wachezaji hao wamebakiza miezi mitatu kila mmoja katika mkataba wake. Wengine ni Haroun Chanongo ambaye yupo Stand United kwa mkopo, Ivo Mapunda, Nassoro Masoud ‘Chollo’ na Joseph Owino.
Awali ilielezwa kwamba Simba hawataendelea na Owino kwani tayari watakuwa wamefikisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni akiwemo mshambuliaji raia wa Kenya Raphael Kiongera ambaye anatarajia kujiunga na kikosi hicho msimu ujao. Kiongera yupo kwao Kenya baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti mwishoni mwa mwaka jana.
Hata hivyo, Mwanaspoti imepata habari za ndani kwamba bado kuna utata kwa upande wa kuachwa kwa Owino kwani tayari kocha ameonyesha kutokubali viwango vya wachezaji wake Simon na Dan Sserunkuma, hivyo lolote linaweza kutokea kati ya wachezaji hao katika usajili wa msimu ujao.

“Unajua kwa sasa viongozi wameegemea upande mmoja tu ambao ni kusaka ushindi katika mechi za Ligi huku wamesahau kwamba baadhi ya wachezaji wao mikataba yao inakwisha na wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu nyingine,” kilisema chanzo chetu.
Simba inapambana kurejesha heshima yake baada ya kutokuwa na matokeo bora kwenye Ligi Kuu Bara katika siku za karibuni.
Previous
Next Post »