MH. PINDA AUNDIWA ZENGWE LA KUTOGOMBEA URAIS



Mhe. Mizengo Pinda
Na mwandishi wetu
mzee wa kimyakimya, a.k.a Mtoto wa Mkulima, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameundiwa zengwe la kutogombea urais licha ya kudaiwa kuanza mbio za kusaka tiketi ya kukiwakilisha Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Vyanzo vya habari vimedai kuwa waziri mkuu huyo amewaambia marafiki zake wa karibu kuwa hatagombea tena nafasi hiyo tamu ya uongozi  kwa kile kilichotajwa kuwa ni kutofurahishwa na mwenendo mzima wa kisiasa ndani ya chama chake.
“Hafanyi harakati za kutafuta uungwaji mkono katika safari ya urais kwa sababu amejitoa kimyakimya, hataki tena,” chanzo kimoja kilidai na kuweka maneno haya kwenye baadhi ya kurasa za mitandao ya kijamii.
Hata hivyo baada ya kuwepo kwa taarifa hizo, wanaomuunga mkono waziri mkuu huyo katika ndoto zake za urais waliibuka na kukanusha habari hizo huku wakieleza kuwa mipango ya kuelekea ikulu bado inaendelea.
“Hili ni zegwe la kumdhoofisha, hajawahi kumwambia mtu kuwa hagombei, kinachoenezwa kwenye mitandao ni kelele za wafa maji wasiomtakia mema Mheshimiwa Pinda, wafuasi tupo na ngoma lazima ikeshe,” alisema Joseph Marwa, mmoja kati ya wachangia mada mitandaoni.
Pamoja na utetezi  huo, bado watengeneza zengwe waliendelea kukoleza hoja kuwa mheshimiwa huyo amefikia uamuzi wa kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa sababu baadhi ya makada wazito ndani ya CCM wamegeuza ugombea urais kuwa uadui badala ya ushindani wa kisiasa.
Madai hayo yamebaki kuwa mizengwe ya uchaguzi mkuu kumhusu waziri mkuu huyo kutokana na mhusika kuendelea kukaa kimya bila kufafanua ambapo washirika wake wamekuwa wakidai kuwa anafanya hivyo kutii maagizo ya chama chake ya kutoanza kampeni mapema na si vinginevyo.
Oktoba, mwaka jana akiwa nchini Uingereza Waziri Mkuu Pinda alimweleza Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Salim Kikeke kuwa anatangaza nia ya urais kimyakimya huku akifafanua kuwa Watanzania ndiyo watakaoamua kama anafaa kushika nafasi hiyo ya juu ya nchi au la!

Previous
Next Post »