VAGINAL PROLAPSE: KULEGEA KWA MISULI SEHEMU ZA SIRI ZA MWANAMKE-3


Dk. A. Mandai
Wiki iliyopita, tulieleza tatizo hili ambalo huwatokea zaidi wanawake walio katika umri mkubwa ingawa pia linaweza kutokea kwa wasichana. Tumeshaeleza chanzo cha tatizo hili na sasa tutaeleza athari zake na tiba kisha tutatoa ushauri.

ATHARI
Licha ya maumivu anayopata mwanamke mwenye tatizo hili, hali ya kulegea kwa misuli ya uke pia humuathiri hata mume kwani naye hushindwa kufurahia tendo la ndoa.
Mama mwenye tatizo la kutanuka kwa uke au kulegea kwa misuli ya uke anaweza kujigundua kwa kufuatilia dalili zote tulizozieleza katika toleo lililopita.
Ni vema unapoona dalili tulizozitaja kwenda kumuona daktari ili akufanyie uchunguzi na kukupa ushauri wa tiba. Vipimo mbalimbali kama kipimo cha damu, vipimo vya ukeni kama vile spectrum examination, kuotesha uchafu wa ukeni, na iwapo mama anasikia maumivu ya tumbo kipimo cha ultrasound kinaweza kutumika kumpima.
Daktari atachunguza mwenendo wa mfumo wa homoni na historia ya tatizo, uchunguzi huo utasaidia kujua kama tatizo ni la kuzaliwa nalo au ni kwa sababu ya uzazi wa karibukaribu na akishagundua tatizo hutoa tiba ambayo huwa zaidi ya moja.

TIBA NA USHAURI
Tiba ya tatizo hili ni kurekebisha misuli hiyo kwa njia ya upasuaji mdogo au kwa kutumia dawa ili kumrudisha mama katika hali yake ya kawaida.

USHAURI
Mwanamke anashauriwa kuepuka kuwa na uzazi wa karibukaribu hivyo afuate uzazi wa mpango kwa kutumia kalenda, sindano, vijiti au kitanzi kama atakavyoelekezwa na wataalamu wa afya kwenye kituo cha tiba.
Mwanamke pia anashauriwa kuepuka kupata magonjwa ya zinaa kama kaswende, kisonono nk. kwani magonjwa hayo yana athari nyingi kama tulivyoeleza awali.
Mwanamke anapohisi ana tatizo hili ukeni, haraka akamuone daktari kwa msaada zaidi wa kimatibabu kwa sababu ni tatizo linalotibika.
Lakini pia mwanamke anashauriwa kula chakula bora hasa mboga za majani ili kuimarisha mwili na kuweka sawa mwenendo wa mfumo wa homoni mwilini mwake.


Previous
Next Post »