Kipa Casillas akata tamaa Simba

Kipa
wa Simba, Hussein Shariff 'Casillas', amekata tamaa ya kurejea uwanjani msimu huu baada ya kushindwa kupona haraka jeraha la upasuaji wa mguu aliofanyiwa kufuatia kuumia wakati wa ziara ya mazoezi nchini Afrika Kusini.
Casillas aliyetua Simba akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro aliumia Desemba mwaka jana wakati timu hiyo ilipokuwa ziarani 'Sauzi' na ana shaka kama ataweza kurejea kabla ya msimu huu kumalizika Mei.
Akizungumza na gazeti hili jana, Casillas, alisema kwa sasa bado anafanya mazoezi mepesi binafsi na uwanjani anakuwa pamoja na timu ya vijana wa umri chini ya miaka 20 (Simba B).
"Bado naendelea na mazoezi, ila sijajua lini nitaweza kurejea uwanjani, siwezi kujua kwa sasa mpaka pale kocha na daktari wa timu watakaposema niko tayari," alisema kipa huyo.
Aliongeza kwamba anaumia kuona ameshindwa kuitumikia Simba kama alivyotarajia wakati anajiunga mwaka jana.
"Ila ndiyo soka lilivyo, naamini nitarejea uwanjani na tena nitakuwa bora kuliko mnavyonifahamu," aliongeza.
Kutokana na Casillas na pia Ivo Mapunda kuwa majeruhi kwa nyakati tofauti, kipa yosso Manyika Peter Jr. amekuwa akianza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambayo sasa iko katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kilitarajiwa kuwasili mkoani Shinyanga jana jioni tayari kuwakabili wenyeji Stand United katika mchezo wa ligi utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Kambarage.
CHANZO: NIPASHE
Previous
Next Post »