Mtoto huyo alinyakuliwa Jumapili iliyopita nyumbani kwao saa 2:15
usiku akiwa amebebwa na mama yake mzazi, Esther Jonathan (30), baada ya
kujeruhiwa kwa kupigwa mapanga usoni, mwili wake ulipatikana baada ya
msako uliofanywa na wananchi.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,
Joseph Konyo, alisema mwili huo ulipatikana juzi saa 12:30 jioni katika
shamba la mahindi lisilo rasmi kutokana na kulimwa ndani ya hifadhi ya
msitu wa Biharamulo, wilayani Chato. Mwili huo ulipatikana kutokana na
jitihada za wananchi walioshirikiana na makachero wa Jeshi la Polisi
baada ya mwananchi mmoja (jina wanalo polisi) kuonekana akikatisha
katika msitu huo, huku upande wa shati lake ukionekana ukiwa na damu.
Kamanda Konyo alisema baada ya raia huyo kuona viashiria hivyo,
alilazimika kutoa taarifa kwa wananchi wenzake, ambao walifuatilia
mwelekeo wa nguo hiyo na kufanikiwa kuona shimo limefunikwa na udongo
mbichi kisha walipofanikiwa kufukua wakauona mwili huo.
“Baada ya wananchi hao kufukua shimo hilo, walifanikiwa kukuta mwili wa mtoto Yohana ukiwa umekatwa mikono na miguu yote...
baadaye mwili huo ulichukuliwa na askari hadi katika Hospitali ya
Wilaya ya Chato kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kamanda Konyo.
Hata hivyo, baada ya kuupata mwili huo, wananchi hao walipandwa na
jazba na kumtuhumu mwananchi huyo kuhusika na mauaji hayo na kuanza
kumshambulia kabla ya polisi kuingilia kati na kumuokoa kutoka mazingira
hayo.
“Hivi sasa tunamshikilia mtu huyo pamoja na baba wa marehemu,
Bahati Misalaba, kwa ajili ya upelelezi zaidi, kwa sasa hatuwezi kumtaja
jina ili kutovuruga uchunguzi wetu,” alisema Kamanda Konyo.
Alisema lengo la jeshi hilo lilikuwa kuhakikisha mtoto huyo
anapatikana akiwa hai, lakini jitihada zao ziligonga mwamba baada ya
kubaini tayari watekaji wamemuua.
Aliwataka wananchi kujiepusha na imani za kishirikina kwa kuwa zinasababisha maafa makubwa na fedheha ndani na nje ya nchi.
“Naomba wananchi watambue hakuna utajiri wala cheo kinachopatikana
kwa kumuua albino. Hizo ni imani za kijinga kabisa. Bali mafanikio
yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa,” alisema Kamanda
Konyo.
Wakati tukio hilo linatokea, baba wa familia, Bahati Misalaba (39)
alikuwa nje ya nyumba yao anaota moto na hakujeruhiwa, huku watoto wake
wengine wawili albino; Shida (11) na Tabu (3) wakicheza nyumba za jirani
na hivi sasa wamehifadhiwa sehemu nyingine.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa, wameingiwa na hofu na kuhusisha
tukio hilo na wanasiasa na wafanyabiashara, ambao hudanganywa na waganga
wa kienyeji kuwa wakitumia viungo vya albino watanyookewa na mambo yao.
Kwa mujibu wa idadi ya waganga wa jadi kwa baadhi za wilaya za
Mkoa wa Geita, ni kubwa sana kwa mujibu wa Afisa Utamaduni Wilaya ya
Geita, Mufungo Paulo, akidai zaidi ya waganga 900 wanatambuliwa wilayani
mwake, wilayani Chato (265) kwa mujibu wa John Katunzi na Bukombe wapo
zaidi ya 600.
Wakati mwili wa mtoto huyo unapatikana, hali ya mama yake mzazi,
Esther, inazidi kuwa mbaya kutokana na hivi sasa kupumua kwa taabu na
mwili kuvimba.
Akizungumza na NIPASHE jana, Dk. Derick David, ambaye ni mkuu wa
kitengo cha dharura katika hospitali ya Rufaa ya Bugando, jijini Mwanza,
alisema hali ya mama huyo inazidi kuwa mbaya kutokana na majeraha
aliyoyapata wakati watu wasiojulikana walipomcharanga mapanga na kumpora
mtoto wake aliyekuwa amembeba.
Dk. David alisema hivi sasa Esther anatumia mipira kwa ajili ya kumsaidia kupumua kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Kutekwa kwa mtoto Yohana, kunafuatia siku ya 54 tangu kutekwa
mtoto mwingine albino, Pendo Emmanuel (4) wa Kijiji cha Ndami, wilayani
Kwimba, mkoani Mwanza, Desemba 27, mwaka jana.
Mpaka sasa pamoja na juhudi za polisi na wananchi, mtoto Pendo hajaweza kupatikana.
Imeandaliwa na Daniel Limbe, Renatus Masuguliko (Chato) na Daniel Mkate (Mwanza).
CHANZO:
NIPASHE
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon