TAS yalaani mtoto albino wa mwaka mmoja kutekwa

Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Tanzania (TAS) kimelaani tukio la kutekwa kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Yohana Bahati , mwenye umri wa mwaka mmoja, katika Kijiji cha Ilelema, Wilaya ya Chato, mkoani Geita.
Mtoto huyo aliibwa mbele ya wazazi wake, Jumapili wiki iliyopita, majira ya saa 2.00 usiku, wakati akiwa amebebwa na mama yake, Esther Bahati (30), baada ya kuvamiwa na kupigwa na mapanga na waporaji, akiwa jikoni.
Kutokana na hali hiyo, TAS imeitaka jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahalifu hao, kwani hawatoki nje ya mkoa huo.
Msemaji wa TAS, Josephat Toner (pichani), alisema mfululizo wa matukio ya kutekwa kwa watoto wenye ualbino nchini unasikitisha sana.
Alisema hadi sasa wakazi wa kijiji cha Ndami, Mkoa wa Mwanza bado wana majonzi kutokana na kutekwa kwa mtoto, Pendo Emmanuel, Desemba 27 mwaka jana, ambaye mpaka sasa hajulikani aliko.
“Leo ni siku ya 52 bado mtoto Pendo Emmanuel hajapatikana, limeibuka lingine. Kweli inasikitisha sana. Tunakosa amani ya maisha yetu, hasa kwa watoto wetu, ambao hawawezi hata kujitetea,” alisema Toner.
Alisema bado kuna haja kwa serikali kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ili kupata uelewa kuwa watu wenye ualbino hawana uhusiano na utajiri, pia iwape ulinzi kutokana na mfululizo wa matukio ya kutekwa.
CHANZO: NIPASHE
Previous
Next Post »