Watoto wa shule wamgomea DC

Zaidi ya wanafunzi 3, 000 wa shule nne za msingi za Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba, Mkoa wa Mbeya, wameandamana na kufunga barabara Kuu ya Tunduma - Sumbawanga na ya Tanzania - Zambia na kusababisha shughuli za  kiuchumi kusimama kwa zaidi ya saa tano katika mji wa Tunduma.
 
Katika tukio hilo, wanafunzi hao walimgomea Mkuu wa Wilaya ya Momba, Abiudi Saideya, alipowaomba watawanyike.
 
Wanafunzi hao kutoka Shule za Msingi Tunduma, Mlimani, Umoja na Mwaka, waliandamana jana kuanzia saa 12:30 alfajiri na kuendelea kukaa barabarani hadi saa 5:40 asubuhi wakiishinikiza serikali kuweka matuta eneo la Mwaka lilikopo barabara kuu ya Tunduma – Sumbawanga jirani na wanakosoma ili kuepusha ajali kuendelea kutokea.
 
Hatua ya wanafunzi kuandamana ilitokana na ajali ya lori lililokuwa likitokea Sumbawanga kwenda Tunduma kuwagonga watatu na kusababisha wawili kufa na mwingine kujeruhiwa vibaya.
 
Mmoja alikufa papo hapo na mwingine wakati akipatiwa matibabu Kituo cha Afya cha mjini Tunduma.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema mwanafunzi Emmanuel Sichone, alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na lori hilo na  Betiel Mbwambwa, alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu kwenye kituo hicho.
 
Kamanda Msangi alisema mwanafunzi, Jackson Sichone amejeruhiwa vibaya na anaendelea kupatiwa matibabu kituoni hapo.
 
NIPASHE ambalo lililikuwa katika eneo hilo, lilishuhudia wanafunzi hao wamekaa barabarani wakiimba nyimbo za kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kufika kusikiliza madai yao.
 
Kabla ya Kandoro kufika, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Saideya aliwasili kwenye eneo hilo.
 
Kabla ya kuzungumza nao,  Diwani wa kata ya Tunduma,  Frank Mwakajoka, alisema eneo hilo ni hatari kwa maisha ya wanafunzi na wananchi tangu barabara hiyo ilipojengwa.
 
Alisema hadi sasa wanafunzi 10 na watu wazima wanane, wamekufa kwa kugongwa na magari, hivyo eneo hilo linahitaji kuwekwa  matuta makubwa.
 
Alisema Januari 15, mwaka huu, alikwenda Ofisi za Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mbeya, kuomba yawekwe matuta eneo hilo, lakini hadi sasa halijatekelezwa.
 
Mwakajoka aliliomba Jeshi la Polisi kuweka askari eneo hilo kuwasaidia wanafunzi kuvuka barabara wakati Tanroads wakiendelea kujenga matuta.
 
Akizungumza na wanafunzi hao, Mkuu wa Wilaya, Saideya,  alisema serikali imesikia kilio chao na itahakikisha matuta yanajengwa ili kudhibiti magari kuendeshwa kwa mwendo wa kasi.
 
Alisema amewasiliana na Tanroads Mkoa wa Mbeya na wataalam wake walikuwa njiani kutoka jijini Mbeya kuja Tunduma kuanza ujenzi wa matuta hayo.
 
“Kuhusu askari kuwapo kwenye eneo hili, naagiza kuanzia sasa askari wa Usalama Barabarani watakuwapo hapa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku kila siku kuhakikisha usalama unakuwapo. Niwahakikishie kuwa matukio haya ya ajali sasa tutayadhibiti,” alisema Saideya.
 
Baada ya kutoa kauli hiyo, Saideya aliwaomba wanafunzi hao watawanyike kurudi shuleni kuendelea na masomo, lakini waligoma huku wakipiga kelele wakisema hawaondoki mpaka kieleweke.
 
Diwani Mwakajoka aliingilia kati na kuwasihi wanafunzi hao ambao walichanganyika na vijana wa mtaani mjini Tunduma watawanyike na kuwakumbusha msiba wa wenzao ambao miili yao ilikuwa bado haijazikwa.
 
Wanafunzi hao walikubali kuondoka barabarani ili kutoa nafasi kwa serikali kutekeleza ahadi zake na kwenda kushiriki maziko ya wenzao waliokufa kwa ajali.
 
Aidha, Mwakajoka alisema kuwa watoe nafasi kwa serikali kuweka matuta hayo haraka na kwamba kama hayatawekwa kwa muda mwafaka, watarudi tena barabarani kuandamana na kufunga njia.
 
Kauli hiyo iliwafanya wanafunzi na vijana wa mitaani kushangilia na kuanza kuondoka barabarani na baada ya muda mfupi magari yaliyokuwa yamezuiwa yalianza kupita kuendelea na safari zake.
 
Tafrani hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri waliokuwa wakitokea Sumbawanga kwenda Mbeya na wale waliokuwa wakitokea Mbeya na mikoa mingine kwenda Zambia, Sumbawanga, Mpanda na Kigoma.
 
 
CHANZO: NIPASHE
Previous
Next Post »