Wakuu wa mikoa, Ma-DC wastushwa Mto Ruaha kukauka

Sasa ni dhahiri kuwa mto Ruaha Mkuu upo hatarini kutoweka kabisa, endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuunusuru.
 
Sehemu kubwa ya mto huo iliyopo katika hifadhi ya taifa  ya Ruaha ambayo imesambaa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Dodoma, imekauka, huku maji yakionekana katika baadhi ya maeneo yametuwama na kutengeneza madimbwi na katika baadhi ya maeneo yakitiririka kwa kasi ndogo tofauti na hali yake ya kawaida yanapokuwapo ya kutosha.
 
Hali ya kukauka kwa mto huo iliwashtua wakuu wa mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya, pamoja na wakuu wa wilaya za Kilolo, Ludewa, Wanging’ombe, Makete na Njombe, waliofanya ziara ya kutembelea maeneo ya mto huo mwishoni mwa wiki, na kujionea jinsi ulivyokauka na wanyama wanavyoathirika kwa kukosa maji katika Hifadhi ya Ruaha.
 
Akizungumza na viongozi hao kabla ya kuanza kwa ziara hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Hifadhi la Kimataifa (WWF) kwa kushirikiana na Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji, Mratibu wa Maji wa WWF, Kevin Robert, alisema lengo ni kuwawezesha viongozi hao ambao mto huo unapita katika maeneo yao kuona kwa macho yao jinsi ulivyokauka ili waweze kuchukua hatua za haraka kuunusuru kuanzia katika maeneo yao. 
 
Alisema kukauka kwa mto huo kunatishia uhai wa wanyama na ekolojia ya Hifadhi ya Ruaha na wananchi ambao wanategemea maji ya Mto Ruaha Mkuu kuendesha shughuli zao za kiuchumi ikiwamo kilimo, kusababisha migogoro ya kugombana rasilimali ndogo ya maji na kushusha uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu yanayotegemea kwa kiasi kikubwa maji ya mto huo.
 
Naye Mhaidrolojia Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Grace Chitanda, alisema kuanzia miaka ya 1994, Mto Ruaha Mkuu umekuwa ukikauka katika eneo la kilomita 120 ndani ya wilaya ya Iringa pekee kila mwaka.
 
Alisema mto huo kwa kiasi kikubwa umeathiriwa na matumizi makubwa ya maji kwa ajili ya shughuli za kilimo, kuingizwa mifugo kwa wingi hasa katika maeneo chepechepe, matumizi ya viwanda, uchimbaji madini, makazi katika vyanzo vya maji kiasi cha kuharibu mikondo ya mto na mabwawa, upandaji wa miti aina ambazo hazihifadhi maji na uendeshai wa mitambo ya umeme usiozingatia hifadhi ya mazingira kutoka katika mabwawa yanayohifadhi maji hali inayohatarisha viumbe hai na hali ya mto.
 
Akitoa taarifa kuhusiana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Dk. Chris Timbuka, alitaja baadhi ya athari za kukauka kwa mto huo kuwa ni binadamu na wanyama kukosa maji, kupungua kwa watalii, mivutano ya kugombea maji, kilimo kudumaa, uzalishaji umeme kupungua,  wanyama kuvamia makazi ya watu maeneo ya jirani kwa ajili ya kutafuta maji na kuharibika kwa ekolojia ya hifadhi na wanyama kufa.
 
Wakizungumza baada kumaliza ziara ya kutembelea mto huo, viongozi hao wakionekana kushtushwa na kile walichoshuhudia, walikubaliana kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo, ikiwamo wakuu wa wilaya kukabiliana na mambo yanayoathiri mtiririko wa maji na kusimamia sheria za utunzaji mazingira katika maeneo yao.
 
Kwa upande wao, wakuu wa mikoa ya Iringa, Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro ambaye aliwakilishwa, walikubaliana kukutana haraka kujadili suala hilo na kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu juu ya suala hilo ambalo waliliita ni janga na baada ya mwezi mmoja wadau wote kukutana kujadili kutafuta njia za kuunusuru mto huo
Previous
Next Post »