Julio: Mwadui FC itamaliza 'Top 3' VPL

Kocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo 'Julio', ametamba kumaliza ndani ya tatu bora ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao baada ya kuipandisha daraja timu hiyo ya Shinyanga.
 
Baada ya miaka 27, Mwadui FC imerejea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kutokana na kumaliza nafasi ya kwanza katika Kundi la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu.
 
Akizungumza na NIPASHE akiwa Shinyanga jana, Julio alisema: "Mimi ni kocha fundi, nimepanda Ligi Kuu na ninakuja kupambana. Siji kushiriki ligi.
 
"Msimu ujao hakuna cha Yanga, Simba wala Azam. Nitamaliza katika nafasi tatu za juu. Tuna timu nzuri na uongozi imara.
 
"Kama Mungu kapanga, kapanga tu. Tulianza kwa kusuasua dhidi ya Panone FC, Toto Africans na Oljoro JKT, lakini baadaye tukawa tunashinda tu.
 
"Ukisikia mtu anaoa ujue kajipanga maana baada ya kufunga ndoa kuna watoto na ada za shule. Kupanda kwetu Ligi Kuu ni sawa na kuoa, tumejipanga kupambana.
 
"Toto ilitusumbua sana maana tulikuwa tunabadilishana nayo kukaa kileleni mwa msimamo," alisema zaidi kocha huyo wa zamani wa Tanzania Stars na Simba.
 
Mwadui FC yenye maskani yake kwenye Migodi ya Almasi ya Mwadui mkoani Shinyanga, imeungana na timu nyingine tatu; Toto Africans ya Mwanza, Africans Sports ya Tanga na Majimaji FC ya Ruvuma kupanda VPL msimu ujao. Timu zote nne ziliwahi kushiriki ligi hiyo.
 
Timu mbili zitakazomaliza nafasi za chini VPL msimu huu, zitashuka daraja kuzipisha timu hizo nne, hivyo kuongeza idadi ya timu shiriki za ligi kuu kutoka 14 hadi 16.
Previous
Next Post »