Na Mwandishi Wetu, Iringa
BADO Mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani hapa haujakaa sawa kufuatia
vifo vya watu 50 waliopoteza maisha kwa ajali ya kontena kudondokea
Basi la Majinja lenye namba za usajili T 438 CED iliyotokea Machi 11,
2015, Uwazi limechimba.
Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Changarawe mjini Mafinga ambapo kontena
hilo lilikuwa kwenye lori la mizigo la Scania lenye namba za usajili T
689 APJ mali ya Kampuni ya Cipex lililokuwa likitokea Dar kwenda Mbeya
huku basi hilo likitokea Mbeya kuelekea Dar.
KILICHOTOKEA BAADA YA AJALI
Kilichotokea baada
ya ajali hiyo ni kuonekana kwa Mkono wa Mungu ambapo mtoto anayekadiriwa
kuwa na umri wa mwaka mmoja mpaka miwili kunusurika katika ajali hiyo
huku watu 50 wakipoteza maisha.
“Mimi naweza kusema ni Mkono wa
Mungu kwa sababu, yule mtoto alikutwa hajaumia popote lakini wazazi wake
wakiwa wamepoteza maisha. Huoni kama ni uwezo wa Mungu mwenyewe?”
alisema askari polisi mmoja aliyekuwa miongoni mwa waliokuwa wakisimamia
zoezi la uokoaji.
WAZAZI WA MTOTO
Akisimulia ilivyokuwa kwa wazazi
wa mtoto huyo ambaye jina lake halijajulikana, mmoja wa abiria
walionusurika, Aidan alisema kuwa, kabla ya kuanza safari jijini Mbeya,
mtoto huyo alibebwa na mama yake akiwa ameongozana na abiria wengine.
“Wazazi wa mtoto waliingia na kukaa siti ya tatu tu kutoka kwa
dereva. Hakuna aliyehisi kwamba mbele ya safari kuna janga kubwa kama
hili.“Basi lilianza safari, kila abiria alikuwa akizungumza na mwenzake,
wengine walikuwa wakiongea na simu. Wapo waliokuwa wakichati, nadhani
ni wale wanaotumia WhatsApp. Kumbe bwana shetani alikuwa anatembea na
sisi,” alisema abiria huyo akiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.
KABLA YA AJALI
Kwa mujibu wa majeruhi mwingine
wa ajali hiyo, baada ya kufika eneo la Changarawe, kwa mbele lilionekana
lori hilo likiwa katika mwendo wa kawaida na hakuna aliyewaza kwamba
litaangukia basi lao.
“Mbele tuliliona lile lori likija, lakini mimi nimekuwa nikisafiri
mara kwa mara kwa kutumia barabara hiyo. Najua eneo hilo lina shimo
lakini sikuwa na wazo kwamba shimo lile litakuwa mtoa roho wa abiria wa
basi letu.
“Wakati tunapishana sasa, lori linapita kulia kwetu, mimi
nilikaa siti ya nyuma upande wa abiria. Ghafla nilishtuka kuona kama
giza linatanda upande wa dereva, mara nikasikia watu wakianza kulia.
“Kabla sijajua ni nini, nikasikia kishindo kikuu. Puuu! Abiria
wengine walisikika wakisema wanakufa, wengine wakiwa kimya! Ndipo
nikajua tumeangukiwa na kontena lakini sikuweza kufuatilia ilikuaje
kwani akili zikawa kama zimeniruka,” alisema abiria huyo bila kutaja
jina lake.
KILICHOMTOKEA MTOTO HUYO
Baadhi ya waokoaji
waliofika mapema mara baada ya ajali hiyo waliliambia Uwazi kwamba,
wakati wanahangaika kuitoa miili ya majeruhi na marehemu, walishangaa
kumkuta mtoto huyo akiwa chini ya siti ya nyuma kabisa maarufu kwa jina
la ‘kwa balozi’, akiwa hana michubuko.
“Baadhi ya abiria walionusurika wakatuambia huyu mtoto alikaa na
wazazi wake kwenye siti ya tatu kutoka kwa dereva. Sasa amefikaje kule
nyuma kwa balozi? Nadhani anayejua ni Mungu.“Unajua watoto wadogo wana
mkono unaowalinda. Mara nyingi katika ajali wao wanasalimika kwa njia ya
ajabu sana,” alisema askari mmoja wakati wa uokoaji.
Picha ya mtoto huyo ilipigwa na mpiga picha Francis Godwin kwenye
Wadi Namba 3 kwa kusaidiwa maelekezo na polisi wa kike na muuguzi mmoja
aliyekuwa na orodha ya watu walionusurika. Watu wengine wawili kitandani
hapo walikuwa ni wasamaria wema waliokuwa wakimsaidia mtoto huyo ambapo
wazazi wake wanasadikiwa walipoteza maisha.
Polisi wakiwa eneo la tukio.
MGANGA MKUU NA MKUU WA MKOA
Juzi, Uwazi
lilizungumza na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Salimin Mahimbo kuhusu
ajali hiyo ambapo alisema mpaka sasa, majeruhi waliolazwa ni saba baada
ya mmoja kufariki dunia na majeruhi mwingine kupelekwa Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya.
“Mpaka sasa tuna majeruhi saba tu, mmoja alifariki dunia. Mmoja
amekimbizwa Muhimbili kwa matibabu zaidi, hali yake si nzuri, hawa saba
wanaendelea vizuri,” alisema Mahimbo.Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina
Masenza alisema mpaka juzi, marehemu wote walishatambuliwa na ndugu zao
na waliolazwa wametambuliwa pia.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon