Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mashehe na Wanazuoni wa Kiislamu, Shehe Khamis Mataka kushoto akizungumza jambo katika picha ya maktaba.
TAASISI ya Mashehe na Wanazuoni wa Kiislamu, imewataka maaskofu nchini wawe wavumilivu, kwani Serikali ni ya watanzania wote.
Aidha,
imewasisitiza watanzania kwa ujumla, kupata elimu ya Katiba
Inayopendekezwa kwa kuisoma kwa makini na kuielewa ili wawe na uwezo na
uhuru wa kuchagua kile wanachokiona kina manufaa kwao, bila kuwepo
shinikizo la kiimani.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana
na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Shehe Khamis Mataka, wakati akitoa tamko
la taasisi hiyo, kufuatia tamko la TCF kuhusu Katiba Inayopendekezwa,
Mahakama ya Kadhi na Hali ya Usalama na Amani ya Nchi.
“Tunawasihi
watanzania wote kuendelea kudumisha undugu wao kama watanzania, bila
kujali rangi, dini, kabila na itikadi za kisiasa na tumkemee yeyote yule
anayetaka kutugawa kwa kutumia misingi ya kidini, kikabila, kisiasa na
kiuchumi” alisema.
Pia, imeiomba Serikali iache kuzingatia tamko
lililotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), badala yake iendelee
na mchakato wa Katiba Inayopendekezwa na Mahakama ya Kadhi kwa kufuata
misingi ya haki.
Shekhe Mataka aliongeza “Taasisi imezipitia kwa
kina nukta zote nne za Tamko hilo pamoja na hitimisho lake na kubaini
kwamba maaskofu wamejisahau kwamba wao ni viongozi wa kiimani na kiroho,
ambao wanatakiwa wawe tayari kumpokea yeyote na kumpa neno la hekima
lililojazwa faraja, bila hata ya kujali itikadi au chama chake cha
siasa.
Badala yake wameamua kutoa faraja kwa
waumini wao kwa kuzingatia utashi wa kisiasa”. “Maaskofu wameamua
kuanzisha utamaduni mpya wa kuendesha mambo ya kisiasa kwa misingi ya
kiimani na hivyo kutoa tishio la kuwagawa watanzania kwa misingi hiyo.
Hivyo baada ya Taasisi yetu kujiridhisha
na yaliyomo katika Tamko hilo la Maaskofu chini ya mwavuli wa TCF,
tunashauri hatua za kuchukua,” alisema.
Alisema, “Kwa kuwa
serikali ina vyombo makini vyenye wataalamu wenye uwezo wa kufahamu na
kuelewa uvunjifu wa katiba na Umoja wa Kitaifa, tunaomba ipuuze tamko
hilo ambalo limeisikitisha taasisi yetu na kuwadhalilisha waislamu.
“Suala la Mahakama ya Kadhi ni haki ya
Waislamu na haliwahusu wala halihitaji ridhaa ya wasiokuwa Waislamu,
kama ambavyo waislamu hawajapata kuombwa ridhaa yao katika yale ambayo
Serikali imekuwa ikiwafanyia wakristo na makanisa yao,” alisema.
Shehe
Mataka alisema, “Taasisi hii inapinga kwa nguvu zote madai ya Maaskofu
kuwa, Waislamu kuwa na Mahakama ya Kadhi ni uvunjifu wa Katiba, kwani
sheria za Kiislamu ni moja ya vyanzo vya sheria ya Tanzania.
Mahakama za Tanzania zimekuwa zikitumia
sheria hizo kuhukumu kesi za waislamu kuhusu ndoa, talaka, mirathi toka
mwaka 1963 na kufuatiwa na sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu ya
mwaka 1964 na kuhitimishwa na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971”.
Alisema,
“Jambo la msingi hapa ni kuwa kesi hizo zinahukumiwa na mahakimu wasio
na elimu, wala ujuzi na sifa za kuwa Makadhi, kwa mujibu wa Sheria za
Kiislamu na ndio msingi wa Waislamu kudai uwepo wa Mahakama ya Kadhi
Tanzania Bara”.
Alisema taasisi hiyo inawakumbusha maaskofu
kuzingatia kuwa madhara ya kuwagawa watanzania kwa misingi ya kiimani,
dhambi yake haitaishia kwenye kadhia ya Mahakama ya Kadhi, wala Katiba
Inayopendekezwa, bali itaendelea kukita mizizi yake katika kila jambo
linalowahusu watanzania.
Mataka alisema, “Jukwaa linasisitiza
viongozi wa dini wabaki kuwa walezi, siyo kuwagawa watu. Mambo ya siasa
tuwaachie wanasiasa, sisi tubaki na heshima yetu ya kuwa viongozi wa
dini, kwa sababu hata waumini wetu wanatuamini tunapoongea jambo kwamba
ni tamko la Kimungu na wanatakiwa kulifuata.
Kwa hili, hata Askofu Mkuu wa Kanisa
Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
ameona hili lina tatizo”.HABARILEO
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon