Mnikulu, Shaban Gurumo, amekiri kupokea mgawo wa zaidi ya Sh. milioni 80.8 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira, unaodaiwa kuwa ni sehemu ya zaidi ya Sh. bilioni 200 zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lakini akasema hata kama asingepata, angeweza kutatua shida zake kwa kuwa anamiliki fedha zaidi ya hizo.
Pia ametaka watu wote, wakiwamo wabunge
na baadhi ya vyombo vya habari waliohusika kutangaza kwamba, alipokea
Sh. milioni 800 kutoka kwa Rugemalira wakati siyo kweli, wachukuliwe
hatua kama zilizochukuliwa dhidi yake, ikiwamo kuhojiwa na kufikishwa
mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kujieleza kuhusiana na
h
Alisema hayo wakati akiongozwa na
wakili wake, Lucas Kamanija, kujieleza kuhusiana na malalamiko dhidi
yake, yaliyowasilishwa na wanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma mbele ya baraza hilo, jijini Dar es Salaam jana.
Gurumo
alidai Rugemalira ni rafiki yake takriban miaka 10 sasa, ndiye
aliyemshauri kufungua akaunti kwenye Benki ya Biashara ya Mkombozi, tawi
la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, kabla ya kumuingizia Sh. 80,
850,000 katika akaunti hiyo.
Alidai aliyemuunganisha na
Rugemalira, ni Dk. Fred Limbanga wa hospitali binafsi ya Sanitas,
iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam, ambaye jana alifika katika baraza hilo
kutoa ushahidi upande wa utetezi.
AMSHANGAA RUGEMALIRA
Hata
hivyo, Gurumo aliliambia baraza hilo linaloongozwa na Mwenyekiti wake,
Jaji Hamisi Msumi, kuwa hakutambua kusudio la Rugemalira kumuwekea fedha
hizo kwenye akaunti hiyo.
Alidai anahisi pengine Rugemalira
alifanya hivyo kwa kuwa kipindi hicho alikuwa ana mgonjwa anayesumbuliwa
na maradhi ya saratani.
Hata hivyo, alidai hakujishughulisha kabisa kuuliza ili kujua sababu za Rugemalira kumuwekea fedha hizo kwenye akaunti yake.
Alidai
aliitwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kuhojiwa na
kutakiwa kwenda na nakala ya taarifa ya benki hiyo, ambayo aliitambua
jana mbele ya baraza hilo.
Hata hivyo, alidai yeye na
Rugemalira hawajawahi kuzungumzia lolote kama fedha hizo ziliwekwa
kwenye akaunti hiyo na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited,
kama hati ya malalamiko ilivyoeleza.
Alidai anafahamu kuwa
kila mwaka mtumishi wa umma anatakiwa kutamka kwenye fomu maalumu ya
ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu mali na
madeni anayomiliki.
Kutokana na hali hiyo, alidai kila mwaka
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa ikimwandikia barua
kumtaka afanye hivyo na kwamba, mara ya mwisho aliyoandikiwa ilikuwa
Oktoba 2, mwaka jana.
Alidai aliwahi kuwasilisha fomu kama
hiyo kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Septemba 29,
ambayo ilipokelewa siku hiyo hiyo na kwamba, tarehe ya mwisho
kuwasilisha tamko kwenye sekretarieti hiyo ilikuwa Desemba 31, mwaka
jana.
Gurumo alidai hajawahi kutumia cheo chake kupata manufaa
kutoka kwa mtu yeyote na pia haijawahi kuingia akilini mwake kuifikiria
kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited.
Pia alidai hajawahi kuwa na uhusiano na Rugemalira wa kiuchumi wala wa kibiashara.
BUNGE, VYOMBO VYA HABARI
Alidai
tuhuma kwamba, alipokea Sh. milioni 800 kutoka kwa Rugemalira, kwa mara
ya kwanza alizisikia redioni zikizungumzwa na Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, bungeni, akiwa ndani ya gari akitokea
nchini Afrika Kusini.
Alidai baadaye tuhuma hizo zilichapishwa kwenye baadhi ya magazeti na katika mitandao ya kijamii.
“Awali,
lilipokuja kwenye Sekretarieti (ya Maadili ya Viongozi wa Umma), cha
kwanza lilikuwa ni Bunge na vyombo vya habari. Kwa sababu hiyo, kama
inaruhusiwa, wahusika wachunguzwe nao wapitie kwenye mikondo hii hii,
ambayo mimi napitia,” alisema Gurumo.
Alidai hata siku moja
hajawahi kuwa na maslahi ya kiuchumi na Rugemalira, mbali na ya kifedha
na pia hana uhusiano wowote na kampuni ya VIP Engineering and Marketing.
Hata hivyo, akihojiwa na Wakili wa Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus, Gurumo alikiri kuwa Rugemalira ni
mmiliki wa VIP Engineering and Marketing Limited.
ADAI KUWA ANA FEDHA NYINGI
Pia
alikiri kuwa taarifa ya benki iliyotolewa ikionyesha aliingiziwa fedha
hizo na VIP Engineering and Marketing iliyowasilishwa katika baraza hilo
na shahidi wa upande wa malalamiko, Basilio Mwanakatwe jana kama
kielelezo, ndiyo aliyoipeleka kwenye kamati ya uchunguzi ya sekretarieti
hiyo ilipomhoji.
Vilevile, akihojiwa na wakili huyo, Gurumo alikiri kutumia fedha alizopewa na Rugemalira kwa matumizi yake binafsi.
“Ningeweza
kufanya hivyo bila kutumia fedha hizo (alizopewa na Rugemalira). Nina
fedha zaidi ya hizo za Rugemalira,” alitamba Gurumo mbele ya baraza hilo
jana.
Alidai kila mfuko wa suruali aliyovaa umesheheni fedha,
hivyo daima maishani mwake hapatwi na ukata kiasi cha kutegemea fedha
za Rugemalira.
“Hapa nina fedha na huku nina fedha,” alisema
Gurumo mbele ya baraza hilo, huku akijipigapiga kwenye mifuko ya suruali
aliyovaa jana.
Hata hivyo, alikana fedha alizopewa na
Rugemalira kuwa zilikuwa ni zawadi na pia alipotakiwa na Wakili Getrude
kueleza kama zilikuwa ni mshahara au posho aliyolipwa na VIP Engineering
and Marketing Limited na siyo zawadi, Gurumo alisisitiza kuwa hajui.
ADAI HAKUJUA FEDHA ZA NINI
Pia
alipotakiwa na Wakili Getrude kueleza kama aliwahi japo tu kujiuliza
sababu ya kupewa fedha hizo, Gurumo alisema hakuwa nayo na kwamba,
tafsiri ya zawadi katika fedha alizopewa na Rugemalira haipo.
Akijibu
swali la wakili mwingine wa upande wa malalamiko, Hassan Mayunga,
Gurumo alidai pia kuwa hakujua kama fedha hizo ni zawadi au manufaa.
Pia
akiongozwa na Wakili Kamanija, Gurumo alidai siyo sekretarieti hiyo tu,
bali hata afisa ma-suul wake, ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais hana
uwezo wa kumpangia matumizi ya fedha na kwamba, Rugemalira hajampa
utaratibu wowote wa kutumia fedha alizompa.
Awali, shahidi wa
upande wa malalamiko, Mwanakatwe, ambaye ni Afisa Uchunguzi, Ofisi ya
Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, akiongozwa na Wakili
Mayunga, alidai alikutana na Gurumo Desemba 19, mwaka jana wakati wa
uchunguzi walioufanya dhidi yake kutokana na taarifa walizozipata kutoka
vyanzo mbalimbali, ikiwamo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Alidai
katika uchunguzi huo, walibaini kuwa Februari 5, mwaka jana, Gurumo
alipokea kiasi hicho cha fedha kupitia tawi la benki hiyo na kwamba,
katika mahojiano, alikiri kupokea fedha hizo.
Kutokana na hali
hiyo, alidai kuwa Gurumo alikiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma
inayokataza kiongozi wa serikali kupokea zawadi zaidi ya awadi
ndogondogo na ukarimu wa kawaida, pia inakataza kiongozi wa umma kudai,
kuomba au kupokea maslahi ya kiuchumi zaidi ya ukarimu wa kawaida au
zawadi ndogondogo.
Alidai kamati ya uchunguzi pia ilibaini
kuwa Gurumo hakutamka zawadi aliyopokea wala thamani yake na
hakuikabidhi kwa afisa mas-uul wake ili amwambie matumizi yake na namna
ya kushughulika nayo.
Shahidi huyo alidai pia kuwa kamati
ilibaini kuwapo na mgongano wa maslahi na kwamba, Gurumo kwa nafasi
aliyonayo serikalini, anafahamu siri nyingi, hivyo kitendo chake cha
kupokea kwa mfanyabishara, ni dhahiri kuwa hakupanga mambo yake namna
ambayo ingemzuia kujiingiza kwenye mgongano wa kimaslahi.
“Viongozi wa umma ndiyo injini ya uendeshaji, wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa viwango, wanapaswa kuonyesha mfano.
Ukiukwaji wa maadili unaweza kuwakosha wananchi imani na serikali yao,” alidai shahidi huyo.
Hata
hivyo, akihojiwa na Wakili Kama shahidi huyo alidai kuwa taarifa
kwamba, Gurumo alipokea Sh. milioni 800 kutoka kwa Rugemalira, hazina
ukweli na ndiyo alihojiwa na kamati ya uchunguzi ya sekretarieti kwa
kuwa hawana utaratibu wa kupokea na ‘kumeza’ porojo.
Mwenyekiti
wa Baraza hilo, Jaji Msumi alizipa pande mbili za shauri hilo muda hadi
Machi 13, mwaka huu, wa kuwasilisha kwa maandishi maelezo yake ya
mwisho kabla ya kuandaa maamuzi na kuyapeleka kwa mamlaka husika za
nidhamu dhidi ya mlalamikiwa.
Leo baraza hilo linatarajia
kusikiliza malalamiko dhidi ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko, anayetuhumiwa kupokea Sh.
milioni 40.4 katika mgawo wa fedha zilizochotwa katika akaunti yailo.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon