Dar es Salaam. Machungu ya Watanzania yakiwa hayajapoa kutokana
na kashfa ya Sh306 bilioni kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow,
ufisadi mwingine wa zaidi ya Sh252 bilioni umeibuliwa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ndani ya
wizara ya ujenzi.
Ukaguzi maalumu uliofanywa na ofisi ya CAG katika
kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12 umebaini kuwa taarifa
iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, bungeni Novemba 2013
kuwa fedha hizo zilitumika kwa miradi ya ujenzi wa barabara, haikuwa
sahihi.
Kutokana na ufisadi huo, habari zilizolifikia
Mwananchi zinasema CAG amependekeza hatua stahiki zichukuliwe kwa
wahusika wa wizara ya ujenzi na wakala wa barabara ili kuleta imani na
uwazi katika bajeti kwa jamii na wahisani.
“Wizara (ya ujenzi) ililidanganya Bunge kuwa kuna
ujenzi wa barabara hizo wakati wakijua kwamba walikusudia kulipa madeni
ya wakandarasi na washauri wa ujenzi wa barabara...mpango mkakati wa
wakala wa barabara wa mwaka wa fedha 2011/12 pamoja na manunuzi
ulioidhinishwa havikuonyesha utekelezaji wa mradi huo,” chanzo cha
habari kilikariri ripoti ya CAG.
Matumizi hayo yasiyo sahihi yaliibuliwa na Kamati
ya Hesabu za Serikali (PAC) Novemba 22, 2013 baada ya kutilia shaka
kiasi hicho cha fedha na ofisi ya CAG kuagizwa kufanya ukaguzi.
Katika kikao hicho ambacho wizara ya ujenzi
iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake wa wakati huo, Balozi Herbert Mrango
alihojiwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe kuhusu hati ya mashaka
waliyoipata kutoka kwa CAG mwaka 2011/12.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya mwaka
huo Sh348.1 bilioni zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililokuwa
limetajwa kuwa ni la mradi maalumu hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa
bungeni.
“Ni vizuri leo (ilikuwa Novemba 22 mwaka 2013)
uiambie kamati fedha hizi ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa
jambo gani. Tunajua kwamba fedha hizi zilipunguzwa Sh95 bilioni na
kupelekwa Wizara ya Uchukuzi, zilibakia Sh252.975 bilioni katika kifungu
hicho lakini kuna bilioni 100 zimetumika visivyo,” alisema Zitto.
Alisema katika majumuisho ya bajeti wizara hiyo,
Dk Magufuli na Dk Harrison Makyembe aliyekuwa Naibu waziri wa wakati huo
aliyekuwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi walitoa
maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha hizo.
Zitto alikariri maneno yaliyorekodiwa kwenye Hansard ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
“Tunaomba fedha Sh252 bilioni kwa ajili ya kuanzia kazi za ujenzi wa barabara.”
“Fedha hizi zitachangia miradi ya wafadhili,” haya
yalikuwa maneno ya Dk Makyembe ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki wakati akifafanua majumuisho.
- Mwananchi
- Mwananchi
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon