Bahanunzi, Mahundi wachezaji bora VPL

Mshambuliaji Said Bahanunzi wa Polisi Moro amechaguliwa kuwa mchezaji bora mwezi Januari wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), huku kiungo mkabaji Joseph Mahundi wa Coastal Union akishinda tuzo hiyo ya mwezi Desemba.
 
Baraka Kizuguto, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wawili hao wamechaguliwa na jopo la makocha kutokana na mchango wao mkubwa kwenye timu zao katika mwezi husika.
 
Kizuguto alisema Mahundi anayeshikilia rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi msimu huu, alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ya Coastal Union mwezi Desemba mwaka jana. 
 
Hata hivyo, mabingwa hao wa 1988 wa Tanzania Bara, walicheza mechi moja tu Desemba wakitoka suluhu dhidi Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya Desemba 27, mwaka jana.
 
Ofisa Habari huyo aliendelea kueleza kuwa Bahanunzi, mfungaji bora wa Kombe la Kagame 2012 (mabao 6) anayechezea Polisi Moro kwa mkopo akitokea Yanga, amekuwa na mchango mkubwa kwa timu yake hiyo mpya tangu ajiunge nayo kwenye kipindi cha usajili cha "dirisha dogo" msimu huu.
 
Mwezi uliopita (Januari), Polisi Moro inayonolewa na Adolf Richard, ilikusanya pointi sita katika mechi nne, ikishinda 1-0 dhidi ya Mbeya City, sare dhidi ya Ndanda FC, Coastal Union na Stand United na kupoteza 1-0 dhidi ya Yanga.
 
Katika mechi hizo, Bahanunzi alifunga mabao mawili yaliyowapa ushindi wa 1-0 nyumbani mjini Morogoro dhidi ya Mbeya City Januari 31 lililoipaisha timu yake hadi katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi, na sare ya 1-1 ugenini mjini Mtwara dhidi ya Ndanda FC Januari 10.
 
"Kwa kuibuka wachezaji bora, Mahundi na Bahanunzi watazawadiwa fedha taslimu Sh. milioni moja kila mmoja kutoka kwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Vodacom Tanzania," alisema Kizuguto.
 
CHANZO: NIPASH
Previous
Next Post »