Ndanda FC yalia njaa

Wabunge wa mkoa wa Mtwara na wadau wengine wa soka wametakiwa kujitolea kwa hali na mali kuisaidia timu ya Ndanda FC ya mkoani hapa inayokabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi ili iweze kupata mahitaji muhimu na kuweza kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
 
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Mtwara (MTWAREFA), Athumani Kambi, wakati alipokuwa akifanya mahojiano maalumu na NIPASHE na kusema kuwa, kwa sasa mbunge wa Mtwara vijijini, Hawa A. Ghasia, ndiyo anayeisaidia timu hiyo.
 
Kambi alisema kuwa tangu wamepanda daraja mpaka hapo walipo sasa hawajapokea msaada wowote kutoka kwa wabunge wengine. 
 
"Sisi tupo na hatuna upande, mbunge akileta msaada tutaupokea,” alisema Kambi na kuongeza kuwa, “sisi mtu yoyote anayetuletea msaada tunatangaza, kwa mfano hivi sasa Mbunge wa Mtwara vijijini analipa posho kwa wachezaji na tunatangaza,” aliongeza.
 
Alisema awali, Mbunge wa Mtwara Mjini, Asnain Murji, alikuwa anatoa mabasi yake kwa kuchangisha kiasi fulani cha pesa kuwasafirisha mashabiki kwenda kuishangilia timu pindi inapokwenda kucheza ugenini lakini kwa sasa huduma hiyo ameisitisha japo alifanya tena hivyo walipokwenda kucheza dhidi ya Yanga Dar es Salaam na kutoka suluhu. 
 
Habari za ndani zinasema Ghasia, ambaye pia ni Waziri wa Tamisemi, anatoa posho kwa wachezaji kila wiki kiasi cha Sh. milioni 1.2.  
 
Kiuhalisia, timu ya Ndanda haijapata matokeo ya kuridhisha katika mechi zake za kwenye uwanja wa nyumbani wa Nangwanda Sijaona isipokuwa mechi moja pekee waliyoshinda 1-0 dhidi ya Azam Novemba 1, mwaka jana.
 
Mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar ilikuwa ni mechi yao ya 15 ya Ligi Kuu msimu huu, na kati ya hizo mechi saba wamecheza nyumbani na kushinda moja tu, mechi tatu wamefungwa ambazo ni dhidi ya Ruvu Shooting 3-1, JKT Mgambo 1-0 na Simba 2-0. Mechi walizotoa sare ni tatu, ambazo ni dhidi ya Polisi Moro 1-1, Stand United 1-1 na Mtibwa Sugar 0-0, na katika msimamo wa ligi wanashika nafasi ya 11 wakiwa na pointi 16.
 
Mechi inayofuata, Ndanda watacheza dhidi ya Coastal Union ya Tanga Februari 21, 2015 kwenye uwanja wao wa Nangwanda Sijaona.
CHANZO: NIPASHE
Previous
Next Post »