Hali si shwari nchini

Dar/Tanga. Ni dhahiri kwamba sasa hali si shwari nchini kutokana na mfululizo wa matukio ya uhalifu ikiwamo kuvamiwa vituo vya polisi, kuuawa kwa polisi na jingine kubwa la juzi la mapigano baina ya polisi wakisaidiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya makundi yanayodhaniwa kuwa ni ya ama ujambazi au kigaidi.
Matukio hayo yanayoliweka Taifa katika wasiwasi zaidi hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, yamekuwa gumzo kila kona ya nchi kutokana na utata wake.
Tukio la Tanga
Katika mfululizo wa matukio hayo, juzi risasi zilirindima mkoani Tanga kwa zaidi ya saa 48 wakati Polisi na askari wa JWTZ waliposhirikiana kupambana na wahalifu hao.
Katika mapambano hayo, askari mmoja wa JWTZ alipoteza maisha na wapiganaji wengine zaidi ya sita kujeruhiwa.
Jana, askari hao waliendelea na operesheni ya kuwasaka watuhumiwa na hadi tunakwenda mitamboni hakukuwa na taarifa zozote za kukamatwa kwao.
Mbali na kutokamatwa watu hao ambao hawajajulikana ni wahalifu wa aina gani, pia silaha zilizokuwa zinasakwa hazikukutwa kwenye Mapango ya Amboni kama ilivyokuwa ikihisiwa, zaidi ya pikipiki moja mbovu na baiskeli tatu. Habari zilizopatikana jana zimedokeza kuwa vikosi vilivyopo katika operesheni hiyo vimebadili mbinu za kuwasaka majambazi hao.
Vilevile, wakazi wa kitongoji cha Karasha Amboni ambao walihama kukimbia mapigano, hadi jana walikuwa hawajarejea majumbani mwao.
Majeruhi
Kwa upande wa majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, wanaendelea na matibabu huku madaktari na wauguzi wakitakiwa kutoa taarifa za kila anayefikishwa hapo akiwa majeruhi.
“Tumepewa maelekezo kwamba kila raia anayefikishwa hapa akiwa na majeraha tutoe taarifa haraka kwa uongozi kwani kuna uwezekano wa kuletwa waliofanya mashambulizi kwenye mapango,” alisema mmoja wa wauguzi kwa sharti la kutotajwa jina.
Wakazi wa Kijiji cha Kiomoni kilicho jirani na mapango ya Amboni, walisema baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikipotosha taarifa juu ya eneo yalikofanyika mapambano, kwamba ni mapango ambayo hutembelewa na watalii na wageni wengine, wakati si kweli


Previous
Next Post »