Sitta amng'oa mteule wa Dk. Mwakyembe.

Ikiwa ni siku 24 tangu Rais Jakaya Kikwete afanye mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameanza kutema cheche baada ya kutangaza kumsimamisha kazi kwa kipindi kisichojulikana Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Madeni Kipande.
 
Kipande aliteuliwa Agosti mwaka 2012 na Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi, baada ya kuwasimamisha kazi vigogo sita wa TPA akiwamo Mkurugenzi Mkuu, Ephraem Mgawe, kutokana na tuhuma mbalimbali za wizi.
 
Baada ya uamuzi huo, Sitta amemteua Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Awadhi Massawe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
 
Dk. Mwakyembe katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Kikwete Januari 25, mwaka huu, alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wizara ambayo alikuwa akiiongoza Sitta.
 
Sitta akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu ya TPA jijini Dar es Salaam, alisema Kipande amesimamishwa kazi kutokana na kukiuka taratibu za manunuzi na zabuni na kuwa na mahusiano mabovu  na wadau wa mamlaka hiyo.
 
“Tumekutana katika kikao cha dharura cha Bodi ya Bandari kutokana na kuzingatia malalamiko ya sehemu mbalimbali kwamba taratibu za zabuni TPA hazikukaa sawa, zinaendeshwa katika namna ambayo hazileti imani, nampongeza Dk. Harrison Mwakyembe alianza vizuri kushughulikia suala hili, lakini bado tatizo halijaisha,” alisema Sitta.
 
“Nimemsimamisha  kazi kwa muda Kaimu  Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Madeni Kipande leo hii (jana) Februari 16, 2015,  ili kupisha  uchunguzi unaohusu tuhuma mbalimbali zinazomkabili,” alisema na kuongeza:
 
“Tuhuma hizo ni pamoja na manung’uniko kuhusiana  na ukiukwaji wa  taratibu  za manunuzi.”
 
Alisema TPA ni kituo muhimu cha uchumi wa nchi kwa sababu karibu asilimia 87 ya mapato yanatoka hapo, hivyo kunahitajika watu kufanya kazi kwa umakini na uadilifu zaidi.
 
Sitta alisema hapakuwapo na uwazi katika zabuni kiasi kwamba hata baada ya Bodi ya Zabuni kufanya maamuzi kumekuwa na ucheleweshaji wa kutoa barua ya kuidhinisha zabuni hizo, hivyo kuleta taswira mbaya kwa serikali.
 
“Kwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande ndiye msimamizi mkuu wa masuala yote ya bandari kuanzia leo, namsimamisha kazi hadi hapo tume niliyoiunda kuchunguza masuala hayo itakapokamilisha kazi,” alisema.
 
Sitta alitangaza kamati aliyoiunda kuchukuza suala hilo kuwa ni Jaji mstaafu Agusta Buheshi ambaye atakuwa Mwenyekiti  na katibu wake ni mfanyakazi wa Wizara ya Uchukuzi, Deogratius Kasinda.
 
Wajumbe wengine ni Dk. Ramadhani Mlingwa ambaye ni Mkurugenzi mstaafu wa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma  (PPRA); Fravian Kinundo (Mkurugenzi mstaafu wa Masoko TPA; Hapiness Senkoro na Mhandisi Samson Luhigo ambao ni wafanyakazi wastaafu wa TPA.
 
Alisema ameamua kuwateua wastaafu katika kamati hiyo ambayo itafanya kazi ya uchunguzi kwa muda wa wiki mbili kwa sababu watu hao hawahitaji cheo.
 
Agosti 24, mwaka 2012,  Dk. Mwakyembe aliifumua TPA kwa kumsimamisha na baadaye kumfukuza  kazi Mgawe na mabosi wengine sita kufuatia tuhuma za ufisadi.
 
Wengine waliosimamishwa ni manaibu wakurugenzi wawili wa TPA ambao ni Julius Mfuko (Maendeleo ya Miundombinu); Hamad Kashuma (Huduma);  Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng’amilo na mameneja wawili wa Bohari ya Mafuta Kurasini Oil Jetty (KOJ) na mhandisi wa bohari hiyo.
 
Dk. Mwakyembe alisema mabosi hao walisimamishwa kwa muda ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazoukabili uongozi wa bandari ukiwamo wizi wa makontena, wizi mkubwa wa mafuta, udokozi wa mizigo na rushwa katika utoaji wa huduma.
 
Alisema kumekuwa na wizi usioisha bandarini kiasi cha kutishia uhai wake kwa kuwa unafukuza wateja ambao wamehamia bandari za Mombasa nchini Kenya na Durban, Afrika Kusini ambako hakuna kero hizo.
 
Hata hivyo, baada ya uchunguzi uliofanywa na kamati aliyoiunda, Dk. Mwakyembe iliwaweka hatiani vigogo hao ambao walifukuzwa kazi rasmi. Hata vivyo, baadhi yao akiwamo Mgawe bado wanakabiliwa na kesi mahakamani
Previous
Next Post »