Tambwe na mastaa wengine wa Simba waliong’ara Yanga

STRAIKA Amissi Tambwe alifunga mabao mawili murua wakati Yanga inaiangamiza BDF XI ya Botswana katika mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika (Caf) juzi Jumamosi.
Tambwe alifunga mabao hayo kwa ustadi mkubwa baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa BDF na kutumia nafasi mbili kubwa alizopata kuleta madhara kwa wapinzani hao na kuiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo ya Afrika.
Mabao hayo mawili ni mwendelezo wa kazi nzuri anayoifanya Tambwe katika kikosi cha Yanga tangu alipojiunga na mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara kwenye usajili wa dirisha dogo, Desemba mwaka jana.
Straika huyo raia wa Burundi alifanikiwa kujiunga na Yanga siku ya mwisho ya dirisha la usajili baada ya kuvunjiwa mkataba wake na Simba aliyokuwa ameitumikia kwa msimu mmoja na nusu. Moja ya mafanikio makubwa ya Tambwe akiwa Simba ni kuibuka mfungaji bora wa msimu uliopita na kuiwezesha timu yake iliyokuwa na mwenendo wa kusuasua kumaliza katika nafasi ya nne.
Kuachwa kwa Tambwe kulizua mjadala mrefu Simba juu ya uhalali wa sakata hilo lakini siasa zilitumika na kudai kuwa straika huyo hana mpya la kuisaidia Simba licha ya kwamba anafanya makubwa Jangwani kwa sasa.

     style="display:inline-block;width:680px;height:300px"
     data-ad-client="ca-pub-3992075039970891"
     data-ad-slot="7646462965">


Achana na Tambwe, Mwanaspoti inakuletea orodha ya mastaa wengine wa Simba waliofanikiwa kung’ara na kikosi cha Yanga.
Kelvin Yondani
Beki wa Kati wa Yanga, Kelvin Yondani naye alijiunga na timu hiyo akitokea Simba ambapo mkataba wake ulimalizika. Taarifa za ndani ya Simba kwa wakati huo zilieleza kuwa, klabu hiyo ilishindwa kumwongezea mkataba Yondani kwa madai ya kushuka kwa kiwango pamoja na kuihujumu timu hiyo. Yondani kwa wakati huo alikuwa amecheza kwa misimu minne mfululizo na Simba na kuwemo kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa wa ligi mwaka 2010 na 2012. Hata hivyo, licha ya madai hayo ya Simba, Yondani amekuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Yanga tangu alipojiunga mwaka 2012 na amekuwa hakosekani katika kikosi cha kwanza cha makocha wote waliopita klabuni hapo. Beki huyo amefanikiwa kutengeneza kombinesheni ya maana na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kuifanya safu ya ulinzi ya Yanga kuwa ya kuogopeka.
Juma Kaseja
Achana na kipa Juma Kaseja aliyetua Yanga mwaka 2013. Hapa anazungumziwa Kaseja aliyetua Yanga msimu wa 2008/09 wakati huo akiwa moto wa kuotea mbali. Kaseja alijiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja kwa kipindi hicho, baada ya kumaliza mkataba wake na Simba na kuwa nguzo muhimu kwenye kikosi cha Yanga kilichotwaa ubingwa msimu huo. Kutua kwa Kaseja kwenye kikosi cha Yanga kwa msimu huo kuliwashtua wengi lakini alirejea Simba baada ya kumalizika kwa msimu, hivyo kuwatuliza mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wameanza kuhamaki.
Emmanuel Okwi
Mshambuliaji Emmanuel Okwi raia wa Uganda aliifungia Yanga bao la kufutia machozi katika kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Simba katika pambano la Nani Mtani Jembe mwaka 2013. Hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza ya Okwi katika kikosi cha Yanga baada ya kujiunga na klabu hiyo katika siku ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo Desemba 15 mwaka huo. Mashabiki wa Simba walikuwa hawaamini kilichotokea hasa baada ya kupata taarifa kuwa mabosi wa klabu yao walikuwa wakihangaika kumrejesha Okwi kundini.
Previous
Next Post »