Katika
kujitetea mbele ya Baraza la Maadili kuhusu tuhuma dhidi yake za
kugawiwa mgawo wa fedha kutoka akaunti ya Escrow, mbunge wa Sengerema
Bwana William Ngeleja alisema kuwa ni kawaida wabunge kupewa misaada na
wafanyabiashara na taasisi za umma. Katika Maelezo yake alirudia tuhuma
dhidi yangu zilizokwisha tolewa huko nyuma kwamba
1) nilipewa fedha na kampuni ya PAP na
2) nilipewa fedha na shirika la NSSF.
2) nilipewa fedha na shirika la NSSF.
Tuhuma zote hizo
nimewahi kuzitolea ufafanuzi na kukanusha kwani hazina msingi wowote na
zilikuwa siasa za majitaka. Hata hivyo bado zimekuwa zikijirudia rudia
kwa malengo maalumu wanayoyajua wanaotoa tuhuma hizo. Watuhumiwa wa
ufisadi wa escrow hawajazoea kuona taasisi za maadili zikifanya kazi kwa
namna ilivyo sasa na hivyo wanajaribu na watajaribu kubwabwaja na
kuhangaika ikiwemo kutaka kila mtu aonekane ni mtuhumiwa kama wao. Ndio
maana Bwana Ngeleja ametaja msururu wa watu wakiwemo wafanyabiashara
kwamba huwapa fedha wabunge bila chembe ya ushahidi.
Hivyo narudia kutamka
kwamba ninataka uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ufanyike mara moja,
wenye ushahidi wapeleke kwenye vyombo vya uchunguzi na niitwe mbele ya
Baraza la Maadili kujieleza. Nikiwa mbunge ambaye maisha yangu yote ya
siasa nimeyatumia kupambana na ufisadi na kuchochea mabadiliko ili
kujenga misingi madhubuti ya uwajibikaji na kuimarisha taasisi zake,
nipo tayari kwa uchunguzi mahususi dhidi yangu dhidi ya tuhuma
zilizotolewa na nyingine zozote ambazo mtanzania yeyote anazo dhidi
yangu.
Naunga Mkono kwa
nguvu kubwa kazi inayofanywa na Baraza la Maadili. Ni kazi ambayo
ilipaswa kuwa imefanyika kwa muda mrefu sana kwa kashfa mbali mbali
ambazo viongozi wa umma wamepata kama vile ile ya rada, rushwa katika
manunuzi ya mafuta mazito kuendesha mitambo ya Umeme, kujipatia mikopo
kwenye taasisi za umma bila kulipa, kujilimbikizia Mali tofauti na
kipato nk. Hivyo naiomba Sekretariat ya maadili iyachukue kwa uzito
maoni ya Bwana Ngeleja na kama yana uzito kwa mujibu wa sheria na kanuni
yafanyiwe uchunguzi. Nipo tayari kufanyiwa uchunguzi.
Katika kujenga
Misingi Madhubuti ya uwajibikaji nchini ni lazima kila kiongozi aheshimu
taasisi kama Baraza la Maadili. Baraza likiendelea kufanya kazi kama
inavyofanyika sasa, vita dhidi ya ufisadi itakuwa imepiga hatua na
porojo za kuzushiana mitaani zitapungua.
Zitto Kabwe
Mwenyekiti PAC
Dar Es salaam, tarehe 4 Machi 2015.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon